DOLA BILIONI 1.3 KUJENGA SGR KIPANDE CHA MAKUTUPORA -ISAKA |Shamteeblog.



Serikali imeandika historia mpya katika sekta ya uchukuzi baada ya kusainiwa mkataba wa Dola za Marekani Bilioni 1.277 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) Lot 3 na 4 kutoka Makutupora hadi Isaka kilometa 368 na Tabora mpaka Isaka 165 na kufanya jumla ya kilometa 533, utiaji Saini huo umefenyika leo tarehe 28 Aprili, 2026 katika Ukumbi wa Treasury Square jijini Dodoma.

Zoezi la utiaji Saini huo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Taasisi za kifedha, mabalozi pamoja na wadau wa maendeleo, huku Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Dkt. Khamis Mussa Omar, akiwa mgeni rasmi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Omar amesema jumla ya mashirika 3 ya fedha kutoka nchi za Italy, Sweden na Poland yamefadhili jumla ya dola Bil. 1.277 kwa ajili ya kuendeleza kipande hicho ambacho utekelezaji wake ulishaanza.

Amesema huu ni uendelezaji wa ujenzi wa Reli hii ya kisasa kwa kuwa kipande cha Dsm- Dom kilishakamilika na kipande cha tano cha isaka-Mwanza mkandarasi yuko kazini huku kile cha sita tabora-kigoma kikiwa kimeshaanza na kusisitiza kuwa ufadhiri huu utaifanya reli ikamilike vipande vyote kwa jumla ya kilometa 2,100

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema kusainiwa kwa mkataba huu wa dola bil. 1.277 ni tukio kubwa la kihistoria litakalowezesha kuibadilisha Tanzania kuwa kitovu cha kisasa cha usafirishaji na usambazaji wa mizigo kikanda na kufungua fursa za biashara

Amesema kuwa tangu kuanza kwa ujenzi wa mradi wa SGR mwaka 2017 zaidi ya km 2,100 ziko katika ujenzi na sehemu ya Dsm-Dom tayari inatumika ambapo imeshasafirisha abiria milioni 5 huku ikisaidia kupunguza muda wa safari na hewa ya ukaa kwa zaidi ya asilimia 50 na kuongeza ajira

Aidha, ameongeza kuwa mradi huu wa SGR Makutupora–Isaka ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuunganisha mikoa ya Tanzania kwa reli ya kisasa na kusisitiza kuwa kukamilika kwake kutafungua fursa mpya za biashara, ajira na maendeleo ya kikanda

Awali Katibu mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba amewashukuru Wadau wa maendeleo kwa ufadhili huo, huku washirika wote wa maendeleo wakiahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali.




By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post