RC PWANI AWASIFU WAFANYAKAZI KWA KUONGEZA TIJA MAHALI PA KAZI |Shamteeblog.

Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge
Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani Mwalimu Susan Shesha
Katibu Tawala mkoa wa Pwani, Bi. Pili Mnyema

***

NA. ELISANTE KINDULU, BAGAMOYO

MKUU wa Mkoa wa Pwani , Bw. Aboubakar Kunenge amewasifu wafanyakazi ndani ya mkoa huo kwa kufanya kazi kwa bidii na kusababisha mkoa kuwa na tija katika mapato serikalini.

Aliyasema hayo alipokuwa akihutubia maelfu ya wafanyakazi wa Sekta ya umma na ya binafsi katika sherehe za Mei Mosi katika viwanja vya Shule ya msingi Mbaruku Wilayani hapa.

RC Kunenge amesema kuwa Kuna wakati Mkoa wa Pwani ulikuwa kati ya mikoa ya chini katika ukusanyaji wa mapato. Lakini kwa sasa mkoa unashika nafasi ya pili ukitanguliwa na mkoa wa Dar es Salaam.

Mkuu wa mkoa huyo amesema ufanisi huo ni kutokana na utumishi uliotukuka uliojaa uzalendo kwa wafanyakazi wa sekta zote katika mkoa wake.

Naye mratibu wa Mei Mosi mkoa wa pwani Mwalimu Susan Shesha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza dirisha la ajira , ujenzi wa madarasa , zahanati, madai yasiyo ya mshahara na huduma zingine za kijamii huku akimpongeza Mkuu wa mkoa huo kwa kusimamia vizuri mkoa na kuhakikisha mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kuwezesha mkoa kuwa na viwanda lukuki.

Mwalimu Shesha pia amewapongeza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya katika mkoa wa Pwani kwa kuitisha mabaraza ya wafanyakazi mapema mwaka huu ikiwa moja ya maagizo ya mkuu wa mkoa huo katika maagizo yake katika sherehe za Mei Mosi za mwaka 2025.

Mwalimu Shesha ambaye pia ni Katibu wa Chama cha walimu Mkoa wa Pwani (CWT) ameiomba Serikali kuangalia maslahi ya watumishi ili mishahara yao iendane na kasi ya kupanda kwa gharama za maisha.

Mwalimu Shesha amezitaja changamoto zingine kuwa ni kwa baadhi ya waajiri kutowapa wafanyakazi mikataba ya ajira, kuwanyima likizo na kutowapa fursa ya kushiriki sherehe za Mei Mosi.

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bi. Pili Mnyema, Mbunge wa Wilaya ya Bagamoyo Mh. Subira Mgalu. Wakuu wa wilaya zote mkoa wa Pwani, Wakurugenzi wa halmashauri, viongozi wa vyama vya wafanyakazi mkoani huko pamoja na wanachama kutoka vyama vya TWICO, TALGWU, CWT, TAMICO , TUGHE, CHODAU na RAWU.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post