MRADI WA VISIMA VYA GESI MNAZI BAY WAONGEZA UZALISHAJI, WANANCHI WANUFAIKA |Shamteeblog.


Mradi wa uchorongaji wa visima vitatu vya gesi asilia unaoendelea katika Kitalu cha Mnazi Bay kilichopo Mkoani Mtwara umeleta manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kufuatia utekelezaji wenye mafanikio.

Mradi huo unaohusisha uchorongaji wa visima viwili vya uzalishaji na kimoja cha utafutaji ulianza kutekelezwa Februari 06, 2026 ambapo hadi kufikia Juni 05, 2026, uchorongaji wa visima viwili vya uzalishaji vilivyopewa majina ya MB5 na MS2 ulikuwa umekamilika na uchorongaji wa kisima cha tatu kilichopewa jina la KASA-1X ulikuwa unaendelea.

Miongoni mwa manufaa yaliyopatikana kufuatia utekelezaji huo ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika Kitalu cha Mnazi Bay ambapo kisima cha MB5 kimeongeza uzalishaji kwa wastani wa futi za ujazo milioni 40 kwa siku na kisima cha MS2 ambacho bado kinafanyiwa majaribio kinatarajiwa kuongeza ujazo mwingine zaidi wa uzalishaji wa gesi asilia.

Ongezeko hili la uzalishaji wa gesi asilia umewezesha uwepo wa gesi zaidi kwa matumizi ya uzalishaji umeme, viwandani, kwenye vyombo vya usafiri (magari na bajaji) na majumbani.

Kwa wananchi, mradi umeleta fursa za ajira na utoaji wa huduma na bidhaa zinazohitajika ambapo zaidi ya watanzania 320 wameajiriwa katika nafasi mbalimbali na kandarasi zanye thamani ya zaidi ya bilioni 20 za kitanzania zimeenda kwa watoa huduma wakitanzania.

Kwa upande wa uwekezaji, utekelezaji wa mradi huu pamoja na miradi mingine ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia inayoendelea umeongeza imani kwa wawekezaji ndani na nje ya nchi kuhusu uhai wa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini

Kukamilika kwa mradi huu wa uchorongaji wa visima vitatu kutaifanya Tanzania kuwa na idadi ya visima 99 vilivyochorongwa tangu kuanza kwa shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini kutoka visima 96 vilivyokuwepo awali.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post