
Na Hadija Bagasha Tanga
Katika juhudi za kuimarisha sekta za utalii na kilimo ambazo ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania, Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga kimeanzisha programu maalumu za elimu zitakazolenga kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na maarifa ya kisasa watakaosaidia kuendeleza sekta hizo na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Hatua hiyo imetangazwa wakati wa Maonyesho ya 13 ya Biashara na Utalii yanayoendelea jijini Tanga, ambapo baadhi ya wahadhiri wa chuo hicho wamesema kuwa uwekezaji katika elimu ya utalii na kilimo ni mkakati wa muda mrefu wa kuandaa rasilimali watu wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya soko la ajira.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dk. Felchesmi Lyakurwa, amesema chuo hicho kimeanzisha programu za ngazi ya cheti na stashahada katika masuala ya kilimo na utalii kwa lengo la kuongeza idadi ya wataalamu watakaoweza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta hizo nchini.
Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii vinavyoendelea kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi, huku Mkoa wa Tanga ukiwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za utalii ambazo bado hazijatumika kikamilifu kutokana na uhaba wa wataalamu wa kutosha katika sekta hiyo.
"Tumefikia uamuzi huu kwa sababu tunahitaji wataalamu wengi zaidi katika eneo la utalii. Mkoa wa Tanga una vivutio vingi vya utalii, na Tanzania kwa ujumla ina hazina kubwa ya vivutio vinavyohitaji wataalamu wenye ujuzi wa kisasa, "
" Kupitia programu hizi, tutatoa vijana waliobobea watakaosaidia kuongeza tija na ushindani katika sekta ya utalii," amesema Dk. Lyakurwa.
Ameongeza kuwa programu hizo zitawajengea wanafunzi uwezo wa kuelewa mifumo ya kisasa ya usimamizi wa utalii, huduma kwa wageni, uhifadhi wa mazingira na matumizi ya teknolojia katika kukuza utalii endelevu.
Kwa upande wa kilimo, Dk. Lyakurwa amesema programu hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya sekta ya kilimo, ambayo inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa nchi na chanzo kikubwa cha ajira kwa Watanzania wengi.
Amesema elimu itakayotolewa itawasaidia vijana kupata maarifa ya kisasa yatakayowawezesha kuwa wataalamu watakaosaidia jamii kuendesha kilimo chenye tija, kuongeza uzalishaji na kutumia teknolojia mbalimbali zinazoboresha sekta hiyo.
"Tunataka kuona vijana wakipata maarifa yatakayowasaidia kuhamasisha na kuendeleza kilimo cha kisasa, chenye tija na kinachoweza kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi," amesema.
Wakati huo huo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dk. Lihoya Chanwali, amesema kuanzishwa kwa Kampasi ya Tanga ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kusogeza huduma za elimu ya juu karibu zaidi na wananchi kwa kuhakikisha vyuo vikuu vinaenea katika mikoa mbalimbali nchini.
Amesema Serikali imekuwa na dhamira ya kuongeza fursa za elimu ya juu kwa vijana wanaohitimu kidato cha sita, na Chuo Kikuu Mzumbe kilipata nafasi ya kuunga mkono jitihada hizo kwa kuanzisha kampasi yake katika Mkoa wa Tanga.
Kwa mujibu wa Dk. Chanwali, uwepo wa kampasi hiyo utaongeza nafasi za udahili kwa wanafunzi wengi zaidi wanaotaka kuendelea na elimu ya juu, huku ukiwa pia ni fursa kwa Chuo Kikuu Mzumbe kupanua huduma zake na kuwafikia wananchi katika maeneo mengi zaidi nchini.
"Uwepo wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga unasaidia kuongeza nafasi kwa wahitimu wa kidato cha sita kujiunga na elimu ya juu.
Aidha, ni fursa kwa chuo kupanua huduma zake na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya elimu nchini," amesema.
Ameeleza kuwa chuo hicho kimeshiriki Maonyesho ya 13 ya Biashara na Utalii kwa lengo la kutoa elimu kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana chuoni, pamoja na kutangaza rasmi ujio wa Kampasi ya Tanga ambayo itaanza kutoa programu za masomo kuanzia ngazi ya cheti, stashahada na shahada.
Mbali na kutoa elimu, chuo hicho pia kinatafuta ushirikiano wa wawekezaji ili kusaidia maendeleo ya miundombinu katika kampasi mpya iliyopo Kijiji cha Gombero, Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga.
Dk. Chanwali amesema eneo linalozunguka kampasi hiyo bado lina fursa nyingi za uwekezaji ambazo hazijatumika kikamilifu, hali inayofungua milango kwa wafanyabiashara na wawekezaji kuwekeza katika huduma mbalimbali zitakazohitajika kadri shughuli za chuo zinavyoongezeka.
Amesema kampasi hiyo inatarajiwa kuanza kwa kudahili wanafunzi wapatao 1,200, lakini kwa sasa uwezo wa mabweni yaliyopo ni kuchukua wanafunzi 360 pekee, jambo linaloacha upungufu wa nafasi za malazi kwa zaidi ya wanafunzi 900.
Kutokana na changamoto hiyo, chuo kinalazimika kuanza shughuli zake kwa idadi ndogo ya wanafunzi wakati kikisubiri upanuzi wa miundombinu ya malazi.
"Iwapo tutapata wawekezaji watakaosaidia kujenga mabweni ndani au nje ya kampasi, tutakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi. Hii pia itasaidia kuongeza shughuli za kiuchumi katika Kijiji cha Gombero na maeneo ya jirani," amesema.
Aidha, amesema kampasi hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa nyumba za wafanyakazi. Kwa sasa chuo kimefanikiwa kujenga nyumba nne pekee, wakati mahitaji halisi yanazidi nyumba 100 kutokana na idadi ya watumishi wanaotarajiwa kufanya kazi katika kampasi hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za chuo, Kampasi ya Tanga inatarajiwa kuwa na wafanyakazi zaidi ya 100, wakiwemo watumishi wa kitaaluma na wasio wa kitaaluma, hali inayofanya uwekezaji katika nyumba za watumishi kuwa moja ya maeneo muhimu yanayohitaji kipaumbele.
Kuanzishwa kwa Kampasi ya Tanga kunatajwa kuwa hatua muhimu si tu katika kupanua wigo wa elimu ya juu nchini, bali pia katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Wilaya ya Mkinga na Mkoa wa Tanga kwa ujumla, kupitia ajira, biashara, uwekezaji na ongezeko la mahitaji ya huduma mbalimbali zinazotokana na uwepo wa taasisi kubwa ya elimu ya juu katika eneo hilo.










By Mpekuzi
Post a Comment