WAZIRI WA KILIMO DANIEL CHONGOLO, AITIKIA WITO WA MBUNGE AZZA KUTEMBELEA SKIMU YA UMWAGILIAJI NYIDA |Shamteeblog.

  


Na Marco Maduhu, Stela Paul, SHINYANGA

Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo, ameitikia wito kwa Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, kwa kutembelea skimu ya umwagiliaji Nyida iliyopo wilayani Shinyanga katika Jimbo hilo.

TAZAMA VIDEO👇👇


Amefanya ziara hiyo leo Oktoba 2,2026 akiwa ameambatana na maafisa mbalimbali wakiwamo kutoka Tume ya Taifa ya umwagiliaji.

Chongolo, akizungumza alipowasili kwenye mradi huo, amemshukuru Mbunge Azza, kwamba kila anapokutana naye amekuwa wakimkumbushia juu ya skimu hiyo ya umwagiliaji Nyida hadi imemuingia kichwani kwake, na amempa msukumo mkubwa kufanya ziara kwenye skimu hiyo ili kujionea mwenyewe kwa macho maendeleo ya mradi huo.
“Mbunge Azza amenipa msukumo mkubwa kucha kwenye mradi huu wa skimu ya umwagiliaji, kila nikikutana na naye lazima ataje nyida na heka zaidi ya 370 nakushukuru sana, ulichokuwa unakisema nimekiona kwa macho,” amesema Chongolo.

Amesema, dhamira ya serikali kuanzisha miradi hiyo ya umwagiliaji imelenga kuweka msukumu wa kupanua kilimo cha uhakika kwa wananchi.
“Mradi huu wa skimu ya umwagiliaji ukikamilika utanufaisha wananchi kwa upande wa Shinyanga 1,500 na Nzega 1,500 jumla wanufaika wote ni 3,000 na hawa ni wakulima tu, lakini watu wengi watanufaika na mradi huu kwa shughuli mbalimbali,” ameongeza Chongolo.

Aidha, ameagiza Mkandarasi ambaye anajenga kivuko kwenye skimu hiyo ya umwagiliaji ,apewa taarifa zake ndani ya wiki tatu juu ya mwenendo wake, kutokana na ujenzi wake kuwa wakusuasua, kwamba amekaa miaka minne, lakini amejenga kwa asilimia 30, na alitegemewa hadi sasa kuwa amefika mbali.
Ameongeza kuwa, jambo la pili watampatia pia taarifa ambazo wamechukua juu ya huyo Mkandarasi, na kwamba anaweza pia kuja mwenyewe kujionea kazi ambayo ameifanya.

“Nataka pia taarifa za Heka 370 mmefanya usanifu, taarifa yake na gharama ya mradi ili tupime uwezo tuangalia mazingira tukubaliane hatua za kuchukua kwa sababu haitakuwa busara tumeweka fedha hapa bilioni 14, tumezuia maji harafu eneo la kulimwa linakwenda kuminywa tena hatupati tija ile ambayo tunaikusudia,” amesema Chongolo.
Awali Mbunge Azza, akizungumza amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwenye mradi huo sh. bilioni 14, na kwamba katika kata hiyo ya Nyida ina vijiji vitatu ambavyo vitanufaika na mradi huo.

“Mheshimiwa Waziri kwenye mradi huu zilikuwa zinatakiwa Hekta 800, ambazo zingeweza kunufaisha wananchi wa Nyida, lakini hadi sasa tunavyoongea na hekta 421 tu, na utakumbuka tu tukiwa Dodoma nilikuja Ofisini kwako nikakueleza kuna Hekta 379 ambazo zimeachwa kwa hiyo kama zile zimeachwa mradi huo hautanufaisha wananchi wa vijiji vitatu tena, ujio wako leo hapa nina amini utasema neno na wananchi hawa wa Itwangi watarudi nyumbani wakiwa na amani ” amesema Azza.
Katika hatua nyingine Azza, amewasilisha pia ombi la wananchi wa kijiji cha Nyida, kwamba wanaomba mashine za kisasa za kuvunia mpunga, “powertiller” na mashine za kupandia mpunga ili walime kitaalamu, pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa barabara kutoka kwenye mradi na kuungana na barabara kuu, na kuomba pia mradi huo ukikamilika Rais Samia Suluhu Hassan afike kuuzindua na uitwe jina lake.

Kufuatia maombi hayo ya Mbunge, Waziri Chongolo, amesema katika dhana hizo za kilimo ni muhimu sana katika eneo hilo na kwamba anaweza pia kuwambia benki ya ushirikia au ya maendeleo ya kilimo kuzungumza nao na kuwapatia mashine hizo na kulipa kidogo kidogo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenziu Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Leopold Runji, amesema mradi huo wa skimu ya umwagiliaji hadi sasa umeshafikia asilimia 94 ya utekelezaji.

TAZAMA PICHA👇👇
Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo (kushoto) akiwa na Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad kwenye mradi wa skimu ya umwagiliaji Nyida.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post