NA DENIS MLOWE, IRINGA
JAMII nchini imeaswa kuzingatia na kuenzi mila, desturi na utamaduni wa ngoma za asili kutoka makabila mbalimbali ya hapa nchini kuliko kuenzi utandawazi ambao unaathiri nidhamu na uzalendo wa vijana wengi.
Kauli hiyo imetolewa na Meya wa Manispaa ya Iringa , Ibrahim Ngwada wakati akizungumza kwenye tamasha la ngoma za asili liloandaliwa na kituo cha radio Cha Nuru fm Cha mjini Iringa katika kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake na kufanyika katika ukumbi wa IDYDC mwishoni mwa wiki.
Ngwada alisema , kizazi cha sasa kimeathiriwa na utandawazi kiasi cha kutishia kuendelea kuwepo kwa uzalendo wa Taifa kwa kuendelea kuiga tamaduni za nje ambazo nyingi haziendani na tamaduni zetu.
Alisema kuwa vizazi vya sasa vinakabiliwa na tamaduni mbalimbali za nje kutokana na utandawazi hivyo wengi kutofahamu tamaduni za ndani ya nchi ambazo zimekuwa zikifikiliwa kwamba ni ushamba.
Alisema kuwa taifa kwa sasa linakabiliwa ombwe la upotofu wa vijana wengi kukosa nidhamu kwa jamii kunakochangiwa kwa kiwango kikubwa na Utandawazi huku jamii inayostahili kuongoza,kusahau misingi ya malezi inayoambatana na kuzingatia mila na desturi za makabila ya Kitanzania.
Ameowamba Watanzania bora wakabadilishana uzoefu wa mila na desturi za ngoma moja hadi nyingine ili kudumisha nidhamu,maadili na uzalendo wa nchi kuliko kuiga masuala yatokanayo na utandawazi ambayo yanaathiri utaifa wetu.
Amekumbusha kuwa utandawazi si mbaya pindi ukitumika kwa masuala ya msingi ya kusukuma maendeleo ya Taifa na si kuiga tamaduni za ughaibuni ambazo ni chanzo cha kuathiri uzalendo wa Watanzania.
Aliongeza kuwa jamii inatakiwa kutambua kwamba ngoma za asili zina mafundisho makubwa katika ujumbe unaotumika kuliko Hali ilivyo kwa Sasa jamaa inakabiliwa uwingi wa tamaduni za nje na wengi wa vijana kukimbilia nyimbo za bongo fleva.
Ngwada alikipongeza kituo cha radio Nuru fm kwa kuweza kukumbuka miaka kumi tangu kuanzishwa kwake kwa namna ya kipekee na kuenzi ngoma za asili.
Katika tamasha hilo Meya Ngwada alitoa zawadi kwa kikundi kilichoibuka kidedea kiasi Cha sh. 300,000 mshindi wa pili alitoa Sh.200,000 na mshindi wa tatu alikipatia sh. 100,000.
Licha ya kutoa fedha hizo mfukoni mwake Ngwada alivikabidhi vikundi vingine 10 vilivyobaki kila kimoja sh.30,000 ikiwa ni Asante kwao kushiriki tamasha Hilo la ngoma za asili.
Kutokana na kuongeza zawadi katika tamasha Hilo kundi la kwanza liliondoka na kiasi Cha 600,000 mshindi wa pili 400000 na mshindi wa tatu aliondoka na 200000 ambazo zilitolewa na waandaji Nuru Fm.
By Mpekuzi
Post a Comment