Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza ujenzi na ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ile iliyopo katika mikoa inayopakana na nchi jirani ili kuharakisha maendeleo ya maeneo hayo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi, alipowaongoza Wajumbe wa mkutano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi kutembelea miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika mkoa wa Kigoma.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Eneo Maalum la Uwekezaji wa Kigoma (Kigoma Special Economic Zone-KiSEZ); Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Bandari Kavu ya Katosho na Bandari ya Kigoma pamoja na Kituo cha Pamoja cha Kutoa huduma Mpakani (OSBP) kinachotarajiwa kujengwa katika eneo la Manyovu mkoani Kigoma.
Akiwa kwenye eneo Maalum la Uwekezaji, Prof. Kabudi na Wajumbe wengine walijionea uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye eneo hilo na Kampuni ijulikanayo kama Next Gen Solar wa kuzalisha umeme wa jua wa megawati tano ambao utaanza kusambazwa rasmi kwa wakazi wa Kigoma mwezi Aprili 2021. Upatikanaji wa nishati hiyo ya umeme unatarajiwa kuwanufaisha wakazi wa mkoa huo kiuchumi.
Kadhalika Mhe. Prof. Kabudi na Wajumbe wengine walipata fursa ya kutembelea kampuni ya Third Man Limited inayozalisha Asali ijulikanayo kama Upendo (Upendo Honey) ambayo nayo imewekeza kwenye eneo hilo maalum la KiSEZ. Katika maelezo yake kwa Mawaziri, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bw. Alex Scovic alisema kuwa Kampuni yake ambayo inachakata asali inayozalishwa bila kutumia kemikali (organic) inanunua asali hiyo kutoka kwa wafugaji wa nyuki zaidi ya 3,000 waliopo Kigoma na mikoa jirani kama Tabora, Katavi, na Rukwa na baadaye kuiuza asali hiyo nje nchi hususan nchini Marekani.
“Kampuni yetu ni ya kwanza kuwekeza kwenye eneo hili. Tunazalisha Asali safi isiyo na kemikali ambayo ina soko kubwa nje ya nchi hususan nchini Marekani. Biadhaa zetu tunazitangaza kuwa zimetoka Tanzania” alisema.
Pia alijulisha kuwa, Kampuni yake imeajiri zaidi ya vijana 60 wa kitanzania na kwamba mbali na kuchakata asali, kampuni hiyo inazalisha nta ambayo huuzwa nchini Ujerumani ambao huitumia kwa ajili ya kutengeneza vipodozi. Kampuni ya upendo huzalisha zaidi ya tani 4,000 za asali kwa mwaka.
Katika ziara yao kwenye eneo la Bandari Kavu la Kitosho, Mawaziri na Viongozi wengine walijulishwa kuwa eneo hilo limeanzishwa maalum kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji na uhifadhi wa mizigo na bidhaa mbalimbali zinazokwenda Burundi kutokea Bandari za Tanzania. Tayari eneo hilo limepata mzabuni atakayeanza ujenzi mwaka huu. Pia Mawaziri hao walitembelea Bandari ya Kigoma na kupata fursa ya kujionea meli kongwe na ya kihistoria ya MV Liemba ambayo ina miaka 108 tangu itengenezwe, MV Mwongozo na MV Sangara ambazo zote zitaanza kufanyiwa ukarabati ili kuziwezesha kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa Kigoma na kutoka nchi jirani.
Wakiendelea na ziara ujumbe huo ulitembelea Uwanja wa Ndege wa Kigoma ambapo ulipata maelezo kutoka kwa Meneja wa TANROAD wa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma kuwa, mradi huo unalenga kupanua na kukarabati maeneo mbalimbali ya Uwanja huo ikiwa ni pamoja na kuongeza urefu wa barabara ya kuruka na kutua ndege ambayo awali ilikuwa na urefu wa mita 1800 na sasa mita 1,300 zitaongezwa ili kuwezesha ndege kubwa kutua. Pia mradi unalenga kujenga jengo la abiria, maegesho ya ndege, usimikaji wa taa na mitambo ya kuongozea ndege, ujenzi wa jengo la kuongozea ndege, maegesho ya magari pamoja na uzio wa usalama.
Mhe. Prof. Kabudi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Balozi Albert Shingiro walihitimisha ziara yao kwa kutembelea eneo kitakapojengwa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Manyovu na Mugina kwa upande wa Burundi. Wakiwa Manyovu waliweza kutembelea maeneo ambayo vituo hivyo vitajengwa kwa upande wa Tanzania na upande wa Burundi pamoja na kupokea taarifa ya mradi huo ambapo walijulishwa kwamba tayari usanifu wa ujenzi wa kituo hicho cha Manyovu ambacho kitakuwa cha aina yake umeanza na utakamilishwa mwishoni mwa mwezi Machi 2021.
Akitoa hotuba kuhitimisha ziara kwenye miradi hiyo, Prof. Kabudi alisema Tanzania inawekeza kwenye miradi hiyo ili kurahisisha ufanyaji biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi mbalimbalii inazopakana nazo ikiwemo Burundi. Kwa upande wake, Mhe. Balozi Shingiro alipongeza jitihada hizo za Tanzania na kuahidi kutumia fursa za miradi hiyo ambayo mingi inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi.
|
Post a Comment