Bondia maarufu wa ngumi za kulipwa Tanzania, Hassan Mwakinyo jioni leo atapanda ulingoni kuwania ubingwa wa uzito wa super welter wa Afrika wa shirikisho la ngumi za kulipwa Afrika (ABU) dhidi ya bondia wa Angola, Antonio Mayala.
Pambano hilo limepangwa kuanza saa 12.00 jioni kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Masaki na mabondia wote wametamba kutwaa mkanda huo ambao upo wazi.
Mwakinyo ambaye ana rekodi ya kushinda mapambano 18 na kupoteza mawili, ametamba kushinda pambano hilo kabla ya raundi ya tano katika pambano hilo la raundi 12.
“Nimejiandaa zaidi ya raundi 12 kwa lengo la kuwa imara muda wote, lengo langu ni kushinda raundi za mwanzoni, lakini nimeamua kumpa nafasi mpaka raundi ya nne au ya tano ili kutoa burudani kwa mashabiki wangu,” alisema Mwakinyo.
Alisema kuwa Mayala hakuwa lengo lake, lakini kwa sababu ameingilia ugomvi wa bondia Brendon Denes wa [MO1] Zimbabwe ambaye ameumia, atatoa kichapo cha hali ya juu.
“Kamwe sitamdharau Mayala kwani ameingilia ugomvi ambao haukuwa wake, atajuta kukubali kupigana na mimi, nitamnyoosha kisawasawa,” alisema.
Alisema kuwa amedhamiria kuwapa furaha mashabiki wake na Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwani atakuwa anapigana kwa mara ya kwanza chini ya uongozi wake.
Mbali ya pambano hilo, bondia mwingine wa Tanzania, Shabani Jongo atawania ubingwa wa uzito wa juu wa ABU dhidi ya bondia kutoka Nigeria Olanrewaju Durodora.
Pambano hilo limepangwa kuwa la raundi 12 na Jongo ametamba kufanya vyema. Katika kusindikiza mapambano hayo mawili, bondia nyota wa Tanzania Ibrahim Class atazichapa na bondia wa Afrika Kusini, Sibusiso Zingange katika pambano la uzito wa light yaliyodhaminiwa na kampuni ya KCB Bank, Plus TV, Multichoice Tanzania, Tanzania Tourism Board, Onomo Hotel, Precision Air, Prestine Logistics, Urban Soul, Global Boxing Stars, M-BET na Epic Sports Entertainment.
Mapambano mengine ya utangulizi yatawahusisha bondia wa Tanzania Daniel Matefu ambaye atazichapa na bondia wa Bulgaria Pencho Tsvetkov ambapo bondia wa kike Leila Yazidu atazichapa dhidi ya bondia mwingine wa Bulgaria Joana Nwamerue.
Pia bondia Hamisi Palasungulu atazichapa na bondia kutoka Congo Brazzaville Ardi Ndembo huku Imani Daudi Kawaya atapigana na bondia kutoka Afrika Kusini Chris Thompson.
Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa alisema kuwa pambano hayo yataonyeshwa katika nchi zaidi ya 32 Afrika kupitia Plus TV ambayo inapatikana kwenye king’amuzi cha DStv.
“Tunajivunia sana kuwa mstari wa mbele kuendeleza vipaji hasa vya ngumi za kulipwa hapa nchini na kushirikiana na serikali. Rumble in Dar 2 ni alama ya maendeleo ya ngumi za kulipwa nchini kwa mujibu wa malengo yetu, tunaomba ushirikiano kutoka kwa wadau, ” alisema Twissa.
Meneja Maendeleo ya Biashara na Miradi wa kampuni ya Jackson Group Sports, Levis Paul akiwatambulisha mabondia Hassan Mwakinyo wa Tanzania (kulia) na Antonio Mayala wa Angola ambao jioni ya leo watapanda kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Masaki kuwania ubingwa wa Afrika wa uzito wa Super Welter. Pambano hilo limeandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sports.
By Mpekuzi
Post a Comment