Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imetoa wito kwa Sekta binafsi nchini kuongeza Vyuo vya ufundi, sayansi na teknolojia ili kuweza kuzalisha wataalamu wengi watakaosaidia Taifa kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama wakati akifungua kongamano la wadau wa mafunzo na ufundi jijini Dodoma leo.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri Mhagama amesema kwa sasa Tanzania ina miradi mingi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere lililopo Rufiji, Pwani, ujenzi wa reli ya Kisasa ya SGRA na ujenzi wa bomba la mafuta linalotoka Hoima Uganda hadi jijini Tanga ambapo miradi yote hiyo inahitaji wataalamu waliobobea kwenye mafunzo na ufundi.
Waziri Mhagama amesema mkutano huo ni mkubwa na wa kipekee kwa kuwa unahusisha wabobezi wa mafunzo ya ufundi ambapo amesema Serikali inaamini kupitia kongamano hilo wabobezi hao watafanya tathimini juu ya ubobezi wa Tanzania kwenye sekta ya mafunzo na ufundi kulingana na mabadiliko ya kiteknolojia duniani kote.
" Huu ni mkutano mkubwa uliohusisha wabobezi wa mafunzo na ufundi nchini kuanzia kwenye ngazi ya umma hadi sekta binafsi, kwa niaba ya Serikali ni imani yetu kuwa kongamano hili litatusaidia kutathmini ule ubobezi wetu kwenye sekta ya mafunzo na ufundi kulingana na hali ya teknolojia hivi sasa.
Niwasihi kila mmoja kujitoa kwa uzalendo wake kwa Taifa letu katika kutoa mawazo na mchango wake katika kuinua tasnia hii ya mafunzo na ufundi,
Nimependa kauli mbiu yenu ya kuwaleta watanzania wote pamoja ikiwemo sekta binafsi na Serikali lengo likiwa kuinua tasnia hii kwa maendeleo makubwa ya ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu kupitia Viwanda," Amesema Waziri Mhagama.
Amesema ulimwenguni kote elimu na mafunzo ya ufundi ndo njia pekee inayoweza kutumika kukuza uchumi akiongeza kuwa maendeleo ya viwanda hayawezi kwenda bila usimamizi bora kwenye vyuo vya ufundi.
Kongamano hilo limeandaliwa na Baraza l Taifa la Elimu ya Ufundi NACTE ambapo kesho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atazindua maonesho ya pili ya elimu yatakayoanza Mei 27 hadi Juni 2 mwaka huu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama akizungumza wakati akifungua kongamano la wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi NACTE jijini Dodoma leo.Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundu Dkt. Adolf Rutayuga akizungumza kwenye kongamano hilo la wadau wa sekta ya mafunzo na ufundi jijini Dodoma.
Washiriki mbalimbali waliohudhuria ufunguzi wa kongamano la wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi lililoandaliwa na NACTE na kufunguliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama.
By Mpekuzi
Post a Comment