WAPINZANI WAMEKUWA WATU WA KULALAMIKA NA KUPINGA MAENDELEO MSIWACHAGUE-MBUNGE KIRUMBA |Shamteeblog.

Charles James, Michuzi TV

ANATOSHA! Ndiyo kauli ambayo ameitoa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Santiel Kirumba alipokua akimuombea kura Mgombea Ubunge wa Jimbo la Buhigwe, Kavejuru Felix katika  mkutano na wananchi wa kata ya Mahinda.

Akizungumza katika mkutano huo Mbunge Santiel Kirumba amewataka wananchi wa Buhigwe kutowachagua wapinzani kwani ni kama watoto wa kambo ambao wamekua hawaridhiki na jambo lolote linalofanywa na badala yake wamekua watu wa kulalamika na kupinga maendeleo.

Amesema wakimchagua Kavejuru wanakua na uhakika wa miradi yao ambayo imeelekezwa kutekelezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwani anakua na uwezo pia wa kumfikia Rais Samia na hata Makamu wa Rais Dk Mpango ambaye anatokea jimbo hilo.

“ Msiwape kura wapinzani wao kila siku ni watu wa kulalamika, ni kama watoto wa kambo ambao wao kila zuri linalofanywa wanasema ni baya, msimpe kura mpinzani kwani hata hajui namna ya kuonana na Rais wala viongozi wengine, huyu Kavejuru yeye akiwa anaomba mjengewe barabara anapiga simu moja kwa moja na inapokelewa.

Naamini Kavejuru anatosha kuwa mwakilishi wenu bungeni wa kuihimiza serikali ijenge barabara hapa, iwaletee vituo vya afya lakini pia ni kiungo baina yenu na serikali katika kuwasemea kwenye miradi ya maji na elimu.

Yaani nyie watu wa Kigoma ni kama mtoto Mziwanda mna bahati Makamu wa Rais anatoka kwenu, mna Waziri wa Elimu, Prof Ndalichako hadi Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Katanga anatoka humu mnataka nini tena watu wa Buhigwe? tuleteeni Kavejuru aungane na hao wengine kusukuma maendeleo kwa wana Kigoma,” Amesema Mbunge Kirumba.

Amewataka wa kina Mama kuwahamasisha wanaume na vijana kuamka alfajiri na mapema kuwahi kwenye vituo vya kupigia kura siku ya Jumapili Mei 16 na kwenda kuichagua CCM ishinde kwa kishindo.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako (kushoto) na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Santiel Kirumba wakimnadi mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Buhigwe Kavejuru Felix.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Santiel Kirumba akipiga magoti kumuombea kura mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Buhigwe, Kavejuru Felix kwenye mkutano na wananchi wa jimbo hilo.
Wananchi mbalimbali waliojitokeza kwenye mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma wakisikiliza Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Santiel Kirumba akimuombea kura Mgombea huyo.

By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post