CHANJO YA UVIKO-19 INA FAIDA NYINGI |Shamteeblog.

Na Joseph Lyimo
KAMA ilivyo kwa nchi nyingine Tanzania imeendelea kuhakikisha mikakati madhubuti ya kujikinga na maambukizi ya janga la UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na utoaji wa chanjo unaendelea kutekelezwa, ikiwemo kueleza faida za chanjo hiyo.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Mariam Seif anasema kuwa elimu inapaswa kutolewa ya kubaini faida inayopatikana pindi mtu akichanja ili kuondokana na dhana potofu.

Mariam Seif anasema tangu chanjo ilipoingizwa nchini kumekuwa na dhana potofu ambazo zimesababisha baadhi ya watu kutojitokeza kuchanja wakidai kuwa chanjo hiyo ya UVIKO-19 ina madhara.

“Kila siku, kila mara na kila wakati unapotaja faida za kupata chanjo ya UVIKO-19, mtu anapata ushawishi wa kuchanja tofauti na kutajiwa na watu wasio wataalamu kuwa kuna madhara pindi mtu akichanja,” anasema.

Mkazi wa kata ya Naisinyai Isaya Lengenyuu anasema kuwa watanzania wanapopatiwa elimu ya faida ya chanjo wanashiriki kwa moyo mmoja tofauti na kuwa na wasiwasi kutokana na watu wasio wataalam kuzusha mambo wasioyajua.

Lengenyuu anataja baadhi ya dhana potofu ya kifo, watu kuwa mazombi au misukule kutokana na chanjo hiyo kushambulia vinasaba, kuvuruga hedhi na kuharibika nguvu za uzazi kwa wanaume na wanawake.

Aloyce Kituyo anasema kuwa faida ya chanjo ya UVIKO-19 ikiwa inaelekezwa kwa jamii mara kwa mara ingekuwa vyema kwa jamii na kuiomba Serikali iendelee kutoa somo hilo kwa jamii.

“Awali watanzania walionyesha wasiwasi kuhusu chanjo ya UVIKO-19 kwenye hatua ya awali za utoaji chanjo na kusababisha mwitikio wa matumizi ya chanjo kuwa hafifu hivyo waelezwe faida za chanjo kila mara,” anasema Kituyo.

Anasema kadiri Serikali inavyotoa elimu ya faida ya kupata chanjo ya UVIKO-19 inavyozidi kutolewa kwa watu, ndiyo elimu inavyozidi kuwaingia na kuondokana na dhana pofotu.

Hata hivyo, wataalam wa afya wamekuwa wakitoa elimu mbalimbali kwa jamii kuwa kuna faida nyingi pindi mtu akipata chanjo ya UVIKO-19 tofauti na yule ambaye hajapata chanjo hiyo.

Mtaalamu wa ufuatiliaji na mdhibiti wa magonjwa wa Wizara ya Afya, Dkt Baraka Nzobo anasema kwamba kuna faida kubwa inayopatikana endapo jamii itashiriki ipasavyo kwenye chanjo ya kujikinga na janga la UVIKO-19.

“Tuendelee kuhimiza watu wote wajitokeze kupata chanjo ya UVIKO-19 maana ndiyo afua muhimu sana katika kukabiliana na janga hili na kuna faida kubwa inayopatikana tofauti na kutochanja,” anasema Dkt Nzobo.

Dkt Nzobo anasema kwamba chanjo ya UVIKO-19 ina faida kubwa mno kwa mtu endapo watashiriki chanjo hiyo tofauti na kutokupata chanjo hiyo na kuingia hofu.

Anataja faida za kupata chanjo ya UVIKO-19 ni kuepusha na kifo endapo mtu amepata maambukizi ya ugonjwa huo na akiwa amepata chanjo hiyo uwezekano wa kifo ni mdogo mno.

Anasema ugonjwa wa UVIKO-19 una haribu nguvu za kiume endapo ukiupata ila ukiwa umeshapata chanjo hiyo na ugonjwa huo ukakukumba, hakuna tatizo litakalokupata kwani chanjo itaepusha na changamoto hiyo pindi ukipona.

“Chanjo ya UVIKO-19 haiharibu nguvu za kiume kwani kirusi cha UVIKO-19 ndicho kinasababisha matatizo kwani ukipata janga hilo na endapo utakuwa haujachanja utapata madhara.

Anasema kuwa endapo mtu akipatiwa chanjo ya UVIKO-19 atakuwa na uhakika wa kuendelea kuwa na nguvu za kiume kwani hata akipata maambukizi hayo hawezi kuathirika kwenye hilo.

“Ujanja ni kuchanja kwa mwanaume na mwanamke hakuna tatizo lolote lile atapata chanjo ya UVIKO-19 na ataweza kupata ujauzito kwani chanjo haileti ugumba kwani utachanja na kupata ujauzito na kuzaa mtoto,” anasema Dkt Nzobo.

Anasema chanjo ya UVIKO-19 inalinda watoto kuathirika kwani watu wazima wakichanja wanakuwa wanawalinda kupata maambukizo ya UVIKO-19 kwani wao watoto wadogo hawachanjwi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akizungumza Agosti 10 mwaka 2022 kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan Mkoani Njombe, anasema janga la UVIKO-19 bado lipo hivyo watanzania na wazee waendelee kupata chanjo ili kujikinga na kupambana.

Waziri Ummy anasema kuwa hivi sasa imedhibitika kuwa chanjo ndiyo njia pekee inayoweza kupunguza makali ya UVIKO-19 na kutengeneza kinga ya jamii hivyo dunia ikaweka malengo ya angalau asilimia 70 ya watu wote kupata chanjo.

Anaeleza kwamba hadi hivi sasa watanzania milioni 15.5 wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea sawa na asilimia 50.53 ya walengwa waliopaswa kupata chanjo wameshiriki kupatiwa chanjo ya UVIKO-19.

Anasema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba watanzania milioni 30.7 wanakadiriwa kupatiwa dozi kamili ya chanjo ya UVIKO-19 hadi mwezi Desemba mwaka 2022.

“Ujanja ni kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani hata ukikumbwa na janga hilo ukiwa umeshapata chanjo hautapambana kwa kutumia nguvu nyingi, tofauti na mtu ambaye hakupatiwa chanjo,” anamalizia kwa kusema Waziri Ummy.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post