Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amebainisha katika kitabu chake kwamba maisha ya wapinzani bungeni yalikuwa magumu kutokana mbinu zilizokuwa zikifanywa na Serikali ya awamu ya tano ya kuwaziba midomo.
Lissu amebainisha hayo kwenye kitabu chake cha “Remaining in the shadows: Parliament and Accountability in East Africa” ambacho alikizindua juzi jijini Nairobi nchini Kenya, hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe.
Katika kitabu hicho, Lissu amefanya uchambuzi wa hali ya siasa na mabunge katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania, huku akielezea mkwamo wa kupatikana kwa katiba mpya nchini.
Lissu ameeleza kwamba katika miaka mitano iliyopita, Serikali ilitumia mbinu mbalimbali kuua nguvu ya upinzani, ikiwa ni pamoja na kuondoa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kwa kisingizo cha kupunguza gharama.
Amesema Serikali ilikuwa na dhana kwamba matangazo ya mijadala ya Bunge yalikuwa yakiwaimarisha wapinzani, hivyo, njia pekee ya kuzuia ikawa ni kusitisha matangazo hayo ili wasipate nafasi ya kutoa mawazo yao.
Lissu alieleza kwamba tishio kubwa kwa upinzani lilikuwa ni kuondolewa kwa uhuru wa kutoa maoni na mijadala bungeni na kwamba hilo lilisababishwa na nguvu kutoka nje ya Bunge.
Amesema mawaziri walikuwa wanapewa hotuba za wapinzani na kuondoa vipengele ambavyo wasingependa visikike wakati wakiwasilisha hotuba yao, jambo ambalo alieleza kwamba limekuwa utamaduni wa Bunge kuwasilisha hotuba katika ofisi ya Katibu wa Bunge siku moja kabla ya kusomwa.
“Vitendo hivi visivyo vya kidemokrasia vilianza siku za mwisho za Bunge la 10 chini ya Spika Anna Makinda, lakini ni katika Bunge la 11 chini ya Spika Job Ndugai ambapo vitendo hivyo vimeshika kasi ya juu,” ameandika Lissu katika kitabu hicho.
Amesema Serikali ilirudisha nyuma hatua ya kidemokrasia iliyopigwa tangu mabadiliko ya sheria ya mwaka 1984. Amebainisha kwamba haki za msingi za kujieleza na kukusanyika, ziliathiriwa sambamba na uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kisiasa wa kujieleza.
Kilio cha katiba mpya
Mbali na masuala ya Bunge, Lissu amegusia kwa kirefu mchakato wa katiba mpya, akisema mchakato huo ulimtegemea Rais pekee kuitisha kura ya maoni baada ya kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa.
Ameandika kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inamtaka Rais kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, kutangaza siku ya kura ya maoni ndani ya siku 14 tangu alipopokea Katiba Inayopendekezwa na kuielekeza tume kuandaa kura ya maoni.
“Rais Jakaya Kikwete hakutumia madaraka yake kuitisha kura ya maoni. Hatuwezi kusema kama alimshirikisha Rais wa Zanzibar au la kuhusu suala hilo. Siyo yeye wala Rais wa Zanzibar aliyezungumza kitu chochote kwa namna yoyote,” amesema Lissu kwenye kitabu chake.
Amesema Rais Kikwete na serikali yake haikuwahi kuweka wazi sababu ya kupuuzia maoni ya Watanzania katika mchakato wa kuandika katiba mpya, jambo ambalo anasema lingemfanya aache urithi kwa vizazi vijavyo.
Uchaguzi Mkuu 2020
Lissu amegusia pia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, na kuonyesha jinsi ulivyotawaliwa na vituko mbalimbali, kama vile kuondolewa kwa mawakala wa vyama vya upinzani, siku ya uchaguzi huku wagombea wengi kuenguliwa bila sababu za msingi.
“Sababu kuu iliyotolewa kwa wagombea walioenguliwa ilikuwa kwamba wagombea wa upinzani wamejaza vibaya fomu zao za uteuzi. Asilimia 96 ya wagombea wa Chadema, chama kikubwa cha upinzani nchini, walienguliwa,” amesema.
Uzoefu wa nchi jirani
Katika kitabu chake, Lissu amechambua pia mchakato wa kuandika katiba ya Kenya ya mwaka 2010.
Pamoja na changamoto za utekelezaji wake, katiba hiyo anasema imeleta mageuzi makubwa katika mfumo wa utawala nchini humo, hasa suala la ugatuzi wa madaraka kwenye kaunti.
Pia, amechambua mfumo wa uendeshaji wa bunge la Uganda na nafasi ya upinzani katika chombo hicho na nchi hiyo ambayo inaongozwa na Rais Yoweri Museveni kwa zaidi ya miaka 30 sasa, na mwaka huu ameapishwa kuendelea kwa miaka mingine mitano.
from Author
Post a Comment