DKT. BITEKO KUZINDUA VIFAA TIBA VYA KISASA HOSPITALI YA NDORAGE KAGERA |Shamteeblog.

Na Lydia Lugakila - Bukoba

Hospitali ya Ndorage, iliyoko katika tarafa ya Kamachumu, Wilayani Muleba, Mkoani Kagera, inatarajia kufanya uzinduzi wa vifaa vikubwa vya kisasa vya tiba kutoka Marekani vyenye thamani ya shilingi bilioni 3 vitakavyozinduliwa na  na Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, tarehe 17 Mei 2025

Akizungumzia kuhusu uzinduzi huo, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dkt. Abednego Keshomshahara, amewataka wananchi wengi kujitokeza kushuhudia tukio hilo muhimu, ambalo linaweza kubadilisha maisha yao kwa kuondoa changamoto za kufuata huduma za matibabu katika mikoa mingine.

Askofu Keshomshahara amesisitiza kuwa vifaa vya tiba vitakavyotolewa vitakuwa na uwezo wa kuchunguza magonjwa mbalimbali ya ndani ya mwili, kama vile majeraha, aina zote za kansa, utafiti wa damu iliyoganda, uchunguzi wa mifupa, na magonjwa mengine makubwa.

 "Hii ni fursa kwa wakazi kazi kwa wananchi wa Mkoani Kagera kuweza kupata huduma bora za afya karibu na nyumbani," amesema mtumishi huyo wa Mungu.

Aidha, Askofu ameongeza kuwa upatikanaji wa vifaa hivi kutasaidia kuondoa changamoto za kutafuta huduma za afya katika mikoa mingine kama Mwanza na Dar es Salaam, pamoja na Nchi za nje. 

Ametoa shukrani kwa serikali kwa kutoa wataalam wa kuhakiki na kuhakikisha vifaa hivyo vinafaa kwa matumizi.

Miongoni mwa vifaa vinavyotarajiwa kuzinduliwa ni pamoja na CT Scan kubwa, X-ray kubwa, Ultrasound kubwa, Digital Mammograph, pamoja na kifaa cha kuchukua picha na kutunza picha  za kuwasiliana na madaktari walioko ndani na nje ya Nchi.

Tukio hili linaonyesha hatua nzuri katika kuboresha huduma za afya katika Mkoa wa Kagera, na kuleta matumaini mapya kwa wananchi wa eneo hilo.



By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post