WANANCHI TEMEKE KUPATA HUDUMA ZA UPIMAJI AFYA NA MATIBABU BURE |Shamteeblog.

* Ni zoezi la 'Temeke Afya Check' lililolenga kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi

MENEJIMENTI ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke wameandaa timu ya madaktari bingwa itakayoendesha zoezi la  upimaji wa afya na matibabu bila malipo kwa wananchi wa Temeke kwa lengo la kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa kadri inavyowezekana.

Akizungumza na Michuzi TV leo jijini Dar es Salaam Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Dr. Joseph Kimaro amesema, zoezi hilo kubwa la 'Temeke Afya Check'  litafanyika katika hospitali hiyo kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba mwaka huu na huduma za upimaji wa afya bila malipo kwa wananchi wote wa Temeke zitatolewa kwa kushirikiana madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya hospitali ya Temeke.

''Hii ni fursa nzuri kwa wananchi wa Temeke kupata huduma za kibingwa na tunafanya zoezi hili kwa lengo la kuhakikisha huduma za kibingwa zinawafikia wananchi wengi kwa kadri inavyowezekana....Tunafahamu wapo wananchi wengi wenye matatizo mbalimbali na wanahitaji kuonana na madaktari bingwa hivyo tukaona tushirikiane na wadau mbalimbali na kutoa huduma hii bila malipo kwa wananchi wetu ili waweze kunufaika na jitihada za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya.'' Amesema. Dr. Kimaro.

Pia amesema gharama za matibabu hayo yatakayotolewa bure kwa wananchi yatagharamiwa na hospitali pamoja na wadau mbalimbali zikiweo kampuni za dawa (Pharmacy) ambao watatoa dawa,  vitendanishi na wataalam pamoja na kulipa gharama za matibabu kwa wagonjwa watakaotakiwa kufanyiwa upasuaji na ushirikiano huo na wadau umelenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali ya kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora ya kuzalisha na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Dr. Kimaro amesema, zoezi hilo limefadhiliwa kwa ukaribu na wadau mbalimbali wakiwemo MDH, Haidery Plaza, Shamshu pharma, MFAA, Nebula, CCBRT, TAI, Consolation Medicare pamoja na Tindwa medical Health ambao watatoa madaktari bingwa wa kutoa huduma katika zoezi hilo, pamoja na wadau wengine wakiwemo NMB, CRDB, Serengeti na NBC ambao pia wameshiriki katika kuhakikisha  wananchi wengi zaidi wanafikiwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya zoezi hilo la 'Temeke Afya Check' na Daktari bingwa wa Kinywa na Meno Dr. Twisibilega Mwakasungule amesema huduma zitakazotolewa bure malipo kuanzia tarehe 9 had 11 Setemba mwaka huu ni pamoja na magonjwa ya wanawake na uzazi, magonjwa ya watoto, magonjwa ya pua, koo na masikio, magonjwa ya mifupa na majeraha ya ajali, magonjwa ya njia ya mkojo na tezi dume, magonjwa ya sukari, figo, shinikizo la damu, magonjwa ya macho na uoni hafifu, magonjwa ya kinywa na meno, upasuaji mkubwa na mdogo pamoja na magonjwa ya akili.

Dr. Twisibilega amesema madaktari bingwa wa magonjwa hayo watakuwepo hospitalini hapo na watatoa huduma na ushauri wa kitaalam na kuwataka wananchi kujitokeza kupata huduma hizo walizosogeza karibu yao bila malipo, na wanategemea kuwahudumia wagonjwa wapatao 5000 ambao wataonana na madaktari bingwa na kupatiwa huduma.

Pia Daktari bingwa wa magonjwa ya macho na mratibu wa huduma za Tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Dr.  Husna Msangi amesema huduma hizo zitatolewa kuanzia saa mbili na nusu asubuhi hadi saa tisa na nusu jioni na wateja wenye bima za afya watapokelewa na kupatiwa matibabu na kueleza kuwa katika katika zoezi hilo watapokea wananchi wanaotumia kadi za bima za afya ikiwemo NHIF.

Awali Daktari bingwa wa upasuaji  na mratibu wa zoezi hilo Dr. Kelvin Rogathe  amesema idara kwa kushiirikiana na wadau wamejipanga kufanya uchunguzi na kutoa matibabu kwa wananchi hasa katika magonjwa ya mdomo sungura kwa watoto, vichwa kujaa maji, majeraha yaliyotokana na moto na henia na wote watachunguzwa na kupatiwa huduma.

Daktari bingwa wa mifupa kutoka hospitali hiyo Dr. Kiandiko Liseki amesema wamejipanga kufanya uchunguzi na kutoa matibabu bure kwa wagonjwa wenye matatizo ya mifupa ikiwemo miguu kufa ganzi, majeraha ya kuvunjika, majeraha  yaliyotokana na ajali ambapo watafanya uchunguzi, kutibu na kuunga mifupa  kwa wagonjwa ambao mifupa yao iliunga vibaya na kupelekea kutembea kusiko sahihi  kwa kuwafanyia upasuaji.

 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Dr. Joseph Kimaro akizungumza na Michuzi TV na kueleza kuwa, zoezi hilo kubwa la 'Temeke Afya Check'  litafanyika katika hospitali hiyo kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba mwaka huu na huduma za upimaji wa afya bila malipo kwa wananchi wote wa Temeke zitatolewa kwa kushirikiana madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya hospitali ya Temeke.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Dr. Joseph Kimaro (kulia,) akiteta jambo na Daktari bingwa wa upasuaji  na mratibu wa zoezi hilo Dr. Kelvin Rogathe (kulia,)  wakati walipozungumzaa na waandishi wa habari kuhusiana na  zoezi hilo kubwa la 'Temeke Afya Check'  litakalofanyika katika hospitali hiyo kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba mwaka huu na huduma za upimaji wa afya bila malipo kwa wananchi wote wa Temeke zitatolewa kwa kushirikiana madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya hospitali ya Temeke.


 



By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post