
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara na kupokea changamoto zinazowakabili Machi 21,2015 katika Kata ya Kishapu Wilayani humo. Picha na Sumai Salum
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara na kupokea changamoto zinazowakabili Machi 21,2015 katika Kata ya Kishapu Wilayani humo.
Na Sumai Salum - Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi amewataka wananchi Wilayani humo kuwekeza elimu kwa watoto wao bila kujali jinsi zao hata ulemavu kwani elimu ndio hazina pekee isiyoibiwa wala kuharibika.
Masindi ameyasema hayo Leo Machi 21,2025 kwenye mkutano wa hadhara wakati akijitambulisha kwa wananchi baada ya kuteuliwa hivi karibuni kuwa mkuu wa Wilaya ya Kishapu ambapo amepokea na kutatua changamoto zinazowakabili huku akisisitiza kuhusu wazazi na walezi kuwapa elimu watoto wao.
"Elimu ni urithi pekee kwa watoto hakikisheni mnasomesha watoto hiyo ndio hazina pekee Mungu amewapa watunzeni,wasomesheni na wala msije mkawatelekeza watoto elimu inalipa Mali huisha ila elimu inadumu hilo mlizingatie sana", amesema Masindi.
Masindi amewataka wazazi na walezi waache tabia za kuwakumbatia watoto waliofikisha miaka zaidi ya kumi na nane kukaa nao majumbani kwani inawalemaza na kutengeneza jamii yenye watu wasio na kipato huku akisema waliofanikiwa ni walioanza kutafuta maisha wakiwa vijana.

Ameongeza kwa kuwataka wanawake,vijana na wenye ulemavu kujiunga na vikundi ili kupata fedha zilizotengwa na serikali kuu zitakazowasaidia kupata mitaji na kuanzisha biashara zenye kuleta tija wabadilishe hali ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na familia zao huku wakikumbuka kuzirejesha fedha hizo kwa wakati.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema tayari serikali imetoa gari la zimamoto na kabla ya mwezi machi kuisha gari hilo litakuwa limefika Kishapu ili kukabiliana na majanga ya moto huku akiwasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya majanga hayo.
"Tuendelee kuchukua tahadhari ya uwepo wa ugonjwa wa Mpox kwa kufuta kanuni za afya na tunao uchaguzi mkuu hapo baadae mwaka huu chagueni viongozi watakaowaletea maendeleo na sio wababaishaji",ameongeza.
Diwani wa Kata ya Kishapu Mhe. Joel Ndettoson amesema mbali na Rais Dkt. Samia kutoa fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo bado kuna changamoto ya vibanda vya kisasa katika gulio la Mhunze,magari ya maji taka,magari ya kubeba taka pamoja na dampo.
"Mhe. Mkuu wetu wa Wilaya tunakushukuru kwani tangia umeletwa Kishapu tunaona unavyoshirikiana na viongozi mbalimbali wakiwemo wataalamu,viongozi wa dini pamoja na wanasisasa na sasa umeamua kuja kuzungumza na wananchi kwa kujitambulisha na kusikiliza changamoto zao tunaamini zitatatuliwa kupitia wewe", ameongeza Mhe. Ndettoson.
Baadhi ya wananchi mbali na kumpongeza kwa uteuzi wake pia wamewasilisha changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ,uwepo wa ajali nyingi Barabara ya Kolandoto Mwangongo,ukosefu wa gari la zimamoto,ukosefu wa machinjio ya kisasa,ukosefu wa choo stand ndogo ya magari(gulioni),chochoro kuzibwa pamoja na ukarabati wa Barabara ya ndani kukarabatiwa kwa kiwango cha rami na kuwekewa taa.

Diwani wa Kata ya Kishapu Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Joel Ndettoson akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Peter Masindi wakati akijitambulisha kwa wananchi na kupokea changamoto zinazowakabili machi 21,2015.
Kaimu Meneja Tarula Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mhandisi Richard Kachwele akijibu hoja na malalamiko ya wananchi waliyowasilisha machi 21,2025 kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Peter Masindi katika Kata ya Kishapu.


Afisa utumishi Wilaya Kishapu Mkoani Shinyanga Tabe Mwananziche akijibu baadhi ya maswali ya wananchi waliyowasilisha machi 21,2025 kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Peter Masindi katika Kata ya Kishapu.

Afisa afya Kata ya Kishapu Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Keneth Mauki akitoa elimu kuhusu ugonjwa Mpox na jinsi ya kuzingatia kanuni za afya kwenye mkutano wa hadhara wa mkuu wa Wilaya hiyo Peter Masindi wakati akizungumza na wananchi na kupokea changamoto zao Machi 21,2025 katika kata ya Kishapu

By Mpekuzi
Post a Comment