Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM katika ziara yake ya kata kwa kata Wilayani Tunduru

Wananchi na wanachama wa CCM wakiwa kwenye mkutano

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akisaini kitabu cha wageni Kata ya Ligoma Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akisalimiana na viongozi wa Chama katika kata ya Tuwemacho

Na Regina Ndumbaro Tunduru .
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Oddo Mwisho, ameendelea na ziara yake ya kata kwa kata, ambapo leo ametembelea kata tatu katika Tarafa ya Namasakata, Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma.
Kata hizo ni Mchuruka, Ligoma, na Tuwemacho Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Oddo amepongeza juhudi za maendeleo zinazotekelezwa na CCM na kuwashukuru wanachama na wananchi kwa kuendelea kukiamini chama hicho.
Aidha, amezungumzia kuhusu kupoteza vitongoji viwili wakati wa uchaguzi uliopita ameeleza kuwa suala hilo limetokana na wagombea wenyewe kutokua makini na utendaji wa kazi katika maeneo yao.
Katika mkutano wake na wananchi, Mheshimiwa Oddo amesisitiza umuhimu wa kupambana na rushwa ndani ya chama.
Amewasihi wanachama kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya viongozi ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi ndani ya chama unakuwa wa haki.
Pia, amezungumzia ucheleweshaji wa pembejeo za ruzuku ya kupulizia korosho (salfa) kwa mwaka huu, akiahidi kuwa ifikapo mwezi Aprili, kila mkulima atahakikishiwa kupokea pembejeo kulingana na hesabu za sensa ya wakulima na mashamba yao.
Mheshimiwa Oddo amejibu maswali yao kwa uwazi na kusisitiza dhamira ya CCM katika kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wote bila upendeleo.
Katika hotuba yake, Mwenyekiti huyo
amekumbusha kuwa viongozi wa chama na serikali wana wajibu wa kuwatumikia wananchi kwa haki na usawa.
Ameeleza kuwa mshikamano kati ya chama na serikali ni nguzo muhimu ya maendeleo ya nchi.
Aidha, amehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza kuwa kupiga kura ni haki yao ya msingi ambayo inapaswa kutumika kikamilifu.
Kwa upande mwingine, Mheshimiwa Oddo amewataka wananchi wa kata ya Mchuruka kuwa watulivu wakati wakisubiri uchaguzi wa diwani mpya, akiwahakikishia kuwa utaratibu wa uchaguzi utafanyika kwa haki.
Pia Mwenyekiti huyo amekemea vikali vitendo vya baadhi ya viongozi wa chama kuleta fujo na vurugu ndani ya chama ili kuvuruga uchaguzi.
Amesisitiza kuwa heshima ya CCM ni jambo la msingi, hivyo kila mwanachama anatakiwa kuheshimu kanuni na taratibu za chama ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mmoja.
Wananchi waliopata nafasi ya kuuliza maswali, akiwemo Rajabu Akili, Bi Aisha Issa, na Jafari Maskini, wameeleza changamoto zao na kushukuru ujio wa Mwenyekiti huyo katika kata zao.
Pia, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wao wa jimbo la Tunduru Kusini Daimu Mpakate kwa jitihada zake za kuwaletea huduma bora za kijamii.
By Mpekuzi
Post a Comment