Naibu Waziri wa Nishati na Mbunge wa Viti Maalumu Vijana Mheshimiwa Judith Kapinga akizungumza na Watumishi wa sekta tofauti ukumbi wa Manispaa Songea Mkoani Ruvuma kuhusu Nishati Safi ya Umeme

Naibu Waziri wa nishati na Mbunge wa Viti Maalumu Vijana Mheshimiwa Judith Kapinga akizungumza na Watumishi wa sekta tofauti ukumbi wa Manispaa Songea Mkoani Ruvuma kuhusu Nishati Safi ya Umeme
Na Regina Ndumbaro Ruvuma .
Naibu Waziri wa Nishati na Mbunge wa viti Maalumu Vijana, Mheshimiwa Judith Kapinga, amezungumzia maendeleo yanayoonekana katika usambazaji wa nishati safi ya umeme nchini, hususan katika Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza leo,katika ukumbi wa Manispaa Songea amesema kuwa Tanzania ina jumla ya vitongoji 64,000, ambapo mpaka sasa vitongoji 33,000 vimepatiwa umeme, huku vitongoji 30,000 vikisubiri kufikiwa.
Aidha, ameeleza kuwa wakati Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, takriban vijiji 4,710 havikuwa na umeme, lakini kwa sasa jitihada zinaendelea kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma hiyo ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kapinga ameeleza kuwa serikali imeanza kutekeleza miradi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji, ambapo Mkoa wa Ruvuma unahusika katika miradi mbalimbali, ikiwemo Mradi wa Ujazilizi na awamu ya kwanza ya utekelezaji wa umeme kwa vitongoji 33,000.
Pia, kuna mradi maalum wa kupeleka umeme katika vitongoji 20. Aidha amebainisha kuwa ndani ya miezi miwili ijayo, kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji 900 itaanza rasmi.
Kwa sasa, Mkoa wa Ruvuma una vitongoji 1,700 ambavyo bado havijafikiwa na umeme, lakini mpango uliopo ni kuhakikisha vitongoji 557 vinapatiwa umeme kwa awamu hii.
Amefafanua kuwa miradi hiyo inazingatia maeneo yenye miundombinu ya umeme na yale ambayo bado hayana miundombinu hiyo, kwa kujenga laini mpya ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika.
Amesisitiza kuwa Mkoa wa Ruvuma ni mkoa wa watu wachapa kazi wanaojihusisha na shughuli za kiuchumi, hivyo upatikanaji wa umeme vijijini utasaidia sana kuanzisha viwanda vidogo na kukuza uchumi wa wananchi.
Serikali imeweka bajeti ya ziada kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa kwa haraka.
Kwa upande wa nishati safi ya kupikia, Kapinga amesema kuwa Mheshimiwa Rais amejikita katika kuhakikisha asilimia 75 ya Watanzania wanapata umeme ifikapo mwaka 2030, na asilimia 80 kufikiwa mwaka 2034 kupitia mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amebainisha kuwa tafiti zilizofanyika mashuleni zinaonyesha kuwa matumizi ya nishati safi yanaokoa gharama kwa asilimia 30 hadi 40 ikilinganishwa na matumizi ya kuni na mkaa.
Kupitia Shirika la Umeme Vijijini (REA), serikali imeshirikiana na Jeshi la Magereza na JKT kusambaza nishati safi, ambapo zaidi ya magereza 300, vituo vya JKT, na shule kongwe 100 tayari zimepatiwa huduma hiyo.
Amezitaka halmashauri za mkoa kushirikiana na serikali katika kutekeleza ajenda hii muhimu, huku akiwashukuru viongozi wa Mkoa wa Ruvuma, wakiongozwa na Kanali Ahmed Abbas Ahmed, kwa juhudi zao katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
By Mpekuzi
Post a Comment